Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

NAIBU WAZIRI KATAMBI AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA MFUKO WA WCF


NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Ajira na Vijana Mhe. Patrobas Katambi amezindua Baraza la Wafanyakazi Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kutoa wito kwa wafanyakazi hao kuchapa kazi kwa bidii kwani ndio nguzo muhimu katika kufanikisha mafanikio ya Mfuko.

Mhe. Katambi ameyasema hayo Mkoani Morogoro leo Februari 10, 2021 wakati akizindua Baraza la Wafanyakazi wa Mfuko wa Fidia (WCF) kwenye ukumbi wa Magadu.

“Lazima tujue uwajibikaji ni nguzo kuu ya mafanikio katika sehemu yoyote ya kazi, hivyo wajumbe mnaowawakilisha wafanyakazi wa Mfuko mnapaswa kuwahimiza wenzenu kuhusu swala hilo.” Alifafanua Mhe. Katambi.

Alisema Serikali inatambua mchango wa wafanyakazi wote nchini lakini vile vile inatambua sana na kuheshimu mchango wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwa kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya wafanyakazi wanaougua au kuumia kutokana na kazi haipotei bali inawapatia huduma ya matibabu au fidia kutokana na tatizo alilopata mfanyakazi katika eneo la kazi.

“Napenda niwahakikishie kuwa Serikali ya awamu ya tano inaendelea kushirikiana na Mfuko huu katika kuhakikisha unanufaisha watu walio wengi na kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwake.”

Naibu Waziri Katambi pia aliupongeza Mfuko huo kwa kuwa na wafanyakazi waliouwezesha Mfuko kupiga hatua kubwa katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Mnatupa heshima kubwa sana ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama tangu mmeanza kutekeleza majukumu ya mfuko kwa mafanikio makubwa, habari hizi zinafurahisha hata kamati ya bunge ilishukuru na kuwapongeza namna mnavyotekeleza majukumu yenu kwa weledi hongereni sana.” Alisema Mhe. Naibu Waziri Katambi.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Bw. Masha Mshomba alisema katika kipindi cha miaka sita ya uhai wa Mfuko kumekuwepo na mafanikio kadhaa ambayo yameweza kutekelezwa vyema na wafanyakazi wa mfuko huo. Sambamba na hilo tumekuwa tukiwapatia mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ujuzi katika utendaji wa kazi.

Bw. Mashomba pia alisema miongoni mwa maeneo ambayo Mfuko umeboresha ni kuwepo kwa mifumo ya utoaji taarifa kwa njia ya mtandao.

“Huduma zetu hivi sasa zinatolewa kwa kiasi kikubwa kwa njia ya mtandao karibu asilimia 85 ya shughuli za mfuko ikiwemo, kujisajili, kuwasilisha michango, uchakataji wa
malipo lakini pia katika kutoa taarifa pale mfanyakazi anapougua au kupata ajali katika maeneo ya kazi au inapotokea bahati mbaya akafariki kutokana na shughuli za kikazi tumeweka mfumo mzuri unaowezesha taarifa hizo kushughulikiwa kwa haraka kupitia mtandao.” Alifafanua Bw. Mshomba.

Alisema Mfuko pia umefungua ofisi za kikanda, kuna ofisi Makao makuu ya Serikali Dodoma, Mbeya, Arusha, Morogoro, Mtwara na mwisho wa mwaka huu wa fedha 2020/2021 Mfuko utafungua ofisi kwenye mikoa ya Tabora, Geita na Shinyanga hususan maeneo ya migodi kama Kahama.