Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Kinga ya Jamii ina mchango mkubwa kwenye uchumi na ustawi wa wananchi - Mhe. Majaliwa


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema huduma ya kinga ya jamii imekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi na ustawi wa wananchi.

Amebainisha hayo leo Aprili 9, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati wa akiwasilisha hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, Mhe. Majaliwa amesema huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwa wananchi ambao ni watumishi walioko kazini, waliostaafu na kaya maskini.

Amesema Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imelipa mafao kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika 23,187 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.17 na pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 175,806 kwa wastani wa shilingi bilioni 72.49 kila mwezi.

Vilevile, amesema kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imelipa mafao ya shilingi bilioni 539.52 kwa wastaafu, wategemezi na wanufaika 110,080 ambapo Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 79.8 zililipwa kama pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 33,840 ikiwa ni wastani wa shilingi bilioni 12 kila mwezi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Majaliwa amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umelipa mafao ya fidia jumla ya shilingi bilioni 7.66 kwa wanufaika wa Mfuko na Kiasi cha fidia kilicholipwa kinajumuisha malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa wanufaika 2,237, kati ya hao wanufaika 516, ni wenye ulemavu, wanufaika 1,692 ni wategemezi na wanufaika 29 ni wanaohudumia wagonjwa wasiojiweza.