News
Waziri Sangu Azindua Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano ya Wadau wa Utatu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amezindua kamati ya kitaifa ya majadiliano baina ya Serikali, Vyama vya Wafanyakazi na Vyama vya Waajiri.
Kamati hiyo imezinduliwa leo Disemba 18, 2025 Jijini Dodoma na Mhe. Sangu ambapo amesema, kamati hiyo ni nguzo muhimu ya mfumo wa mahusiano ya kazi na ajira unaozingatia haki, wajibu na maslahi ya kila mdau.
Kamati hiyo ni jukwaa la kimkakati litakalowezesha kujenga Imani na mawasiliano ya wazi, kukuza tija, ubunifu na ushindani wenye haki, kuzuia na kutatua migogoro ya kazi kwa njia ya majadiliano, kuimarisha mahusiano mema baina ya Serikali, Waajiri, Wafanyakazi na jamii.
Aidha, amesema kamati hiyo inatekeleza kwa vitendo Sheria za Kazi, Ajira, Sheria ya Utumishi wa Umma na viwango vya kimataifa vya kazi vya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambavyo Tanzania inaviridhia.
Vile vile, amesema uzinduzi wa kamati hiyo ambayo uanzishwaji wake unatekeleza misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan haki ya kufanya kazi katika mazingira salama na ya haki, kushirikiana na kushiriki katika maamuzi yanayogusa maslahi ya kijamii na kiuchumi.
Awali akizungumza Mwakilishi wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Said Wamba, ambaye pia ni Katibu Mkuu CHODAU amesema TUCTA itaendelea kushirikiana kwa karibu katika kujenga mazingira ya amani na utulivu baina ya Waajiri na Wafanyakazi, hali itakayochochea ufanisi kazini na kuimarisha mahusiano ya kikazi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba amesema kamati hiyo ni muhimu kwa wadau wa sekta ya kazi na ajira kujadili fursa ana changamoto zinazojitokeza na kuzitatua kwa wakati, hatua itakayosaidia kudumisha amani na utulivu mahali pa kazi.
Amesisitiza kuwa mbinu hiyo itawezesha sekta ya kazi na ajira kufikia malengo na matarajio waliyojiwekea kwa manufaa ya waajiri, wafanyakazi na taifa kwa ujumla.
