Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndejembi aitaka TUCTA kutoa elimu ya Vyama vya Wafanyakazi sekta zisizo rasmi


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi Vijana Ajira na wenye Ulemavu), Mhe Deogratius Ndejembi amewataka viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kuweka mipango madhubuti ya kuwafikia na kuwapa elimu wafanyakazi wanaofanya kazi katika sekta zisizo rasmi ili waone umuhimu wa kujiunga katika vyama hivyo.

Mhe Ndejembi ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wakuu wa vyama vya wafanyakazi vinavyoratibu sekta zisizo rasmi ambapo amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na sekta hiyo kwa kuwa ni nyenzo kuu inayosukuma ukuaji wa uchumi wa nchi.

“ Nitoe rai kwenu viongozi mnaohudhuria mafunzo haya kuyatumia vizuri kuwafikia wafanyakazi waliopo kwenye sekta isiyo rasmi ili waweze kujiunga na vyama hivi. Wapeni elimu ya namna gani watanufaika na kujiunga na vyama. Serikali inawatambua na inathamini kazi kubwa wanayoifanya,” Amesema Mhe Ndejembi.

Amesema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha sekta hiyo inapata mitaji ili kuzidisha ongezeko la wajasiriamali wengi na kukuza biashara zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw Hery Mkunda amesema lengo la mafunzo hayo kwa viongozi hao ni kuwapa uwezo, maarifa na fursa mbalimbali ambazo wafanyakazi wa sekta zisizo rasmi wanaweza kuzipata ambapo matarajio makubwa ya mafunzo hayo ni kuona wafanyakazi kutoka sekta isiyo raski wanajiunga na vyama vya wafanyakazi.