Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI YADHAMIRIA KUENDELEA KUKUZA UJUZI KWA VIJANA NCHINI


Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kukuza ujuzi kwa vijana kupitia Programu ya ukuzaji ujuzi ili kusaidia nguvukazi hiyo ya taifa kupata ujuzi stahiki utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Ameeleza hayo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukagua maendeleo ya mafunzo ya Uanagenzi katika Chuo cha VETA, Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alieleza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilianzisha Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa lengo mahususi la kuipatia nguvukazi ya Taifa ujuzi na stadi za kazi ili waondokane na changamoto ya ajira.

“Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inayolenga kuwezesha nguvukazi ya taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira,” alisema

“Katika siku Mia Moja za Uongozi wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kuwa vijana waendelee kupatiwa mafunzo hayo ya stadi za kazi na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga bajeti kwa ajili ya kuwezesha vijana zaidi kupatiwa ujuzi kupitia programu hiyo,” alisema Mhagama

Alifafanua kuwa katika utafiti uliofanyika wa nguvukazi mwaka 2014 ulibainisha idadi kubwa ya nguvukazi iliyokuwa kwenye ajira takribani asilimia 79.9 ina kiwangi cha chini cha ujuzi na asilimia 16.6 ina kiwango cha kati cha ujuzi ambapo asilimia 3.6 ina kiwango cha juu cha ujuzi.

“Utafiti ulibainisha Nguvukazi tuliyonayo nchini ambayo zaidi ya asilimia 56 ikiwa ni vijana ujuzi wao ni mdogo, hivyo serikali iliweka malengo ya kuanzisha Programu ya kukuza ujuzi ili kuwafikia vijana zaidi na kutatua tatizo la ajira pamoja na kuwezesha nguvukazi hiyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa,” alieleza Mhagama.

Aliongeza kuwa, Programu hiyo inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu umekuwa na mifumo bora ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiri vijana wenzao mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo kwa kuwa wanakuwa na ujuzi wa kutosha katika fani walizopatiwa ujuzi.

Waziri Mhagama aliwapongeza Vijana wa Kike kwa kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa hiyo iliyotangazwa na serikali. Sambamba na hayo aliwasihi vijana walionufaika na mafunzo hayo ya Uanagenzi kuwa na bidii.

“Nimefurahi kuona kundi kubwa la Wanawake wamejiunga katika fani mbazo hapo awali zilikuwa zinaonekana za wanaume tu, lakini leo nimeshuhudia katika madarasa yenu fani za Ufundi wa Umeme wa Majumbani, Ufundi Vyuma, Uchomeleaji na Uungaji Vyuma, Useremala, Terrazzo, n.k wanawake nao wamejiunga kwenye fani hizo,” alisema

Aidha, Waziri Mhagama ameagiza uongozi wa Vyuo vya VETA kuanzisha kanzi data itakayokuwa na taarifa za vijana hao wanaosoma fani mbalimbali ili watakapo hitimu mafunzo yao waweze kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kiuchumi zitakazo wawezesha kuanzisha shughuli au miradi itakayowakwamua kiuchumi.

Kwa upande wake Kijana Mnufaika wa Mafunzo hayo Bi. Mwanaidi Lulomba ameishukuru Serikali kwa kuwapatia vijana fursa hiyo ya mafunzo katika fani mbalimbali na kueleza kuwa ujuzi waliopata utawasaidia kuondokana na changamoto ya ajira.