News
Ridhiwani Kikwete azindua Bodi ya Wadhamini PSSSF
*Aitaka Bodi kusimamia uwekezaji wenye tija
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua Bodi ya wadhamini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) leo Machi 27, 2025, jijini Dar es Salaam.
Aidha, ameitaka Bodi hiyo kuhakikisha inasimamia uwekezaji wenye tija wa Mfuko huo na mipango ya kutoa huduma bora kwa wanachama.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Bodi hiyo, Mhe. Waziri Kikwete ameelekeza Bodi hiyo kusimamia Sera, Sheria, Kanuni sambamba na kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ili watendaji wa mfuko waendelee kuwajibikaji kwa uadilifu, ubunifu na ushirikiano katika kazi.
"Misingi hii ni muhimu kwa sababu inahakikisha PSSSF inafanya kazi kwa ufanisi, usawa na haki, kuepuka rushwa kwa watumishi na viongozi katika kuhakikisha Mfuko unakua endelevu na kukuza uhimilivu wake," amesema Mhe. Kikwete
Akitoa shukrani, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Joyce Mapunjo ameshukuru uteuzi wa wajumbe wa Bodi hiyo ambazo utawezesha ustawi wa Mfuko.
"Wajumbe wa Bodi hii uteuzi wake umezingatia taaluma zote muhimu, kumekua na mchanganyiko mzuri tunaamini kazi tuliyopewa tutatekeleza vizuri," alisema Bi. Mapunjo.
Vile vile, Mwenyekiti wa Bodi hiyo amemuhakikishia Mhe. Waziri kuwa Bodi mpya imepokea maelekezo yote aliyotoa na kuahidi kuyafanyia kazi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru amesema Mfuko utatia ushirikiano mkubwa kwa wajumbe wa kamati ili kufanikisha malengo ya mfuko.