Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Rais samia apongezwa kwa kuwakwamua kiuchumi Vijana na Wenye Ulemavu


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imempongeza Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuhakikisha makundi mbalimbali ikiwamo vijana na watu wenye ulemavu yanajikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.

Akizungumza leo Januari 20, 2025 katika kikao cha kamati jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Fatuma Toufiq amesema wameona jitihada hizo za Mhe. Rais kupitia utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na programu ya ukuzaji ujuzi kwa vijana zinasaidia wananchi kufikia malengo.

Aidha, amesema Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umewezesha vijana kupata mitaji ya kuendeleza ama kuanzisha miradi ya uzalishaji mali. Pia Mfuko wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu ambao umewezesha kundi hilo kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mhe. Toufiq amepongeza jitihada za serikali za kuwawezesha vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana na kuwashauri wadau wengine ikiwamo kampuni kubwa nchini zishirikishwe kuchangia kutunisha mfuko huo ili vijana wengi wanufaike.

Kuhusu huduma zinazotolewa kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira chini ya ofisi hiyo (TaESA), Mwenyekiti huyo ameshauri kasi iongezwe ya kupeleka taarifa kwenye vyuo kuhusu fursa zilizopo za ajira kwa vijana.

Kwa upande mwengine, amepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kuandaa Mfumo wa kitaifa wa taarifa za soko la ajira utakaorahisisha upatikanaji wa takwimu za ajira.

Awali, akitoa ufafanuzi wa hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameahidi kufanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati kwenye suala la ajira kwa vijana na kuongeza kasi ya ufatiliaji wa marejesho ya fedha za mikopo iliyotolewa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana.

Vile vile, amesema Ofisi hiyo imekuwa ikiwawezesha vijana kupata ujuzi ili kupambana kwenye soko la ajira kupitia mafunzo ya uanagenzi.