Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Rais Samia anatambua changamoto za Wenye Mahitaji maalum - Mhe. Majaliwa


WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa leo Machi 24, 2025 ameshiriki futari na watoto wenye mahitaji maalum wa shule ya msingi Buigiri iliyopo Chamwino Mkoani Dodoma inayomilikiwa na kanisa la Anglikana Tanzania.

Akizungumza na watoto hao Mheshimiwa Majaliwa amewaeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto za watu wenye mahitaji maalum na mara zote anawezesha utatuzi wake.

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwaasa watoto wenye mahitaji maalum nchini kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo yao "Tumieni nafasi ya kuwa hapa kusoma sana, wasikilizeni walimu wenu, wako kwa ajili yenu"

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaunga mkono taasisi za dini kaunzisha maeneo ya kuwahudumia watanzania kwenye sekta mbalimbali za huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kufufua vyuo sita vya watu wenye ulemavu ambavyo vilikuwa vimefungwa kwa zaidi ya miaka kumi.

Mheshimiwa Katambi amesema Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya ukarabati wa vyuo hivyo "Pia Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vingine vipya vya watu wenye ulemavu na tumeanza ujenzi kwenye mikoa ya Mwanza, Ruvuma na Kigoma,"