Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Prof. Ndalichako Apongeza PSSSF kwa Kutekeleza Agizo la Rais Samia


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan la kulipa wastaafu mafao kwa wakati.

Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo Februari 2, 2023 mjini Morogoro alipokuwa akizindua Baraza la pili la wafanyakazi wa mfuko wa PSSSF.

“Mlitumie baraza hili kuhimiza kila mfanyakazi ajue wajibu wake ili kuuwezesha mfuko kusonga mbele katika kutekeleza maagizo ya serikali pamoja na kutoa huduma bora kwa wanachama,”amesema.

Aidha, amesema Mhe.Rais ameendelea kushughulikia changamoto za wastaafu ikiwa ni pamoja na kuwataka watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kulipa mafao watumishi walioondolewa kazini kwa kubainika kuwa na vyeti feki.

“Kulikuwa na jumla ya watumishi Elfu Kumi na Nne (14,000) ambao waliondolewa kwenye utumishi kwa sababu ya vyeti feki, tayari watumishi 6,892 wameshalipwa na 3,169 bado madai yao yanafanyiwa kazi,” Alifafanua.

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba, amesema kwasasa mafao hayo ya wastaafu wanalipwa ndani ya siku 60 na uhakiki wa wastaafu unafanyika kidigitali.