Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mkakati wa Kutokomeza Utumikishwaji Watoto Wazinduliwa


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imezindua Mkakati wa Pili wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto unaolenga kuimarisha uratibu wa jitihada zinazofanywa na wadau pamoja na mifumo ya taarifa zitakazo baini utumikishwaji wa watoto.

Aidha, amesema matarajio ya serikali kupitia mkakati huo wa mwaka 2024/25 - 2028/29 suala la utumikishwaji wa watoto litapungua kwa kiwango kikubwa ambapo ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Mkakati huo ili kufia malengo yaliyokusudiwa.

Naibu Waziri Ofisi hiyo Mhe. Patrobas Katambi Juni 12, 2024 amesema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto, yaliyofanyika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.

Mhe. Katambi amesema Tanzania imeridhia Mikataba ya Kimataifa inayohusu ulinzi wa haki za watoto, ikiwemo Mkataba ya Shirika la Kazi Duniani Na. 138 unaohusu Umri wa chini wa mtoto kuajiriwa na Mkataba Na. 182 unaohusu Kazi hatarishi kwa Mtoto.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Fauzia Ngatumbura, ametoa wito kwa Jamii na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya utumikishwaji wa watoto kwa kutoa taarifa za watu wanaowaajiri na kuwatumikisha watoto.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Glory Emmanuel ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa msitari wa mbele katika kupinga vitendo vya utumikishwaji dhidi ya watoto na kuahidi kuendeleza sera, mikakati na programu za kupinga utumikishwaji wa watoto.