Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Halmashauri Zatakiwa Kuchimba Visima vya Maji kwa Kilimo Kitalu Nyumba


Kamati ya Kudumu ya Bunge Ustawi na Maendeleo ya Jamii imezitaka Halmashauri zote nchini kuchimba visima vya maji kwa ajili ya mradi wa mafunzo ya kilimo kwa vijana kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (Green House).

Kuchimbwa kwa visima kutasaidia kuondoa changamoto ya maji hususani katika maeneo yanayokabiliwa na ukame ili kuendeleza mashamba darasa na kunufaika na programu hiyo.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatuma Toufiq Machi 18, 2023 Wilayani Meru Mkoani Arusha baada ya kamati hiyo kutembelea mradi huo ulioanzishwa mwaka 2021/22 kwa ajili ya kutoa elimu kwa vijana na kuwakwamua kiuchumi.

Mhe. Toufiq ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kuandaa programu ya vitalu nyumba vya maua kwa vijana kutokana na hitajio kuwa kubwa kitaifa na kimataifa.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Riziki Lulida ameishauri ofisi hiyo kuandaa vitalu nyumba kwa watu wenye ulemavu ili kuwapatia ajira za kudumu na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Naibu Waziri Ofisi ya Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema gharama za ujenzi wa vitalu nyumba saba Mkoani Arusha vimegharimu Sh. Milioni 294,165, 185.

Mhe. Katambi amesema katika kutengeneza mazingira wezeshi kwa vijana vitalu nyumba vimekabidhiwa Mikoa 17 katika Halmashauri kama sehemu ya kuendelea kutoa elimu kwa uratibu wa Mkurugenzi na Afisa Maendeleo ya jamii kwa maeneo husika.

Naye, mnufaika wa mafunzo hayo Iggu Wilfrey ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kutoa mafunzo kwa vijana ambayo yamewasaidia kujiinua kiuchumi kwa kuweza kusafirisha bidhaa ya pilipili nchini uingereza.

Licha ya mafanikio hayo, Wilfrey amesema wameendelea kutoa elimu kwa vijana wengine ambapo kupitia elimu hiyo wanaitwa sehemu mbalimbali kwa ajili ya kujenga vitalu nyumba ikiwemo TARI na Moshi ushirika.

Sambambana hayo ameiomba serikali kuwapatia eneo la kutosha kwa ajili ya uzalishaji kutokana na mahitaji kubwa la bidhaa linalohitajika katika soko la kimataifa.