Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Dkt. Mpango: Tutasimamia Demokrasia na Amani Uchaguzi Mkuu 2025


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kusimamia kwa dhati misingi ya demokrasia.

Akizindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2025 katika Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa serikali zitahakikisha wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba kushiriki uchaguzi kwa uhuru, kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuchagua viongozi wenye sifa wanaowataka katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Amewataka wananchi, hususan vijana, kuwa waangalifu na kuepuka kutumiwa vibaya na watu wasioitakia mema nchi kwa kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani huku akihimiza wadau wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa, kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha kampeni zinaendeshwa kwa staha na kwa kuzingatia sheria na miongozo ya uchaguzi ili kudumisha amani na utulivu nchini.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zitumike kuwaelimisha wananchi kuhusu haki yao ya msingi ya kushiriki uchaguzi mkuu kwa maendeleo ya Taifa. Alisisitiza kuwa kila Mtanzania anahusika katika mchakato wa uchaguzi na kushiriki kwa amani ni muhimu, kwani bila amani hakuna maendeleo.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema kuwa tangu kuasisiwa kwake na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961, Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chachu ya mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umasikini, pamoja na kichocheo cha maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru utatembelea miradi 64 yenye thamani ya Sh.Trilioni 1.24 katika halmashauri tisa za mkoa huo, kwa lengo la kuwaletea wananchi huduma bora za maendeleo.