Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Kikwete azindua miradi yenye thamani ya Shilingi Bil. 1.6 Wilayani Songwe


Wananchi wamshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha za miradi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi , Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua miradi ya Elimu, Umeme na barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 katika Halmashauri ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe

Akiongea wakati wa uzinduzi wa Miradi hiyo leo tarehe 24 Februari 2025, amesema Mradi wa Ujenzi wa shule ya Maweni B ambao umegharimu shilingi milioni 583 utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule kwa watoto wa Mkwajuni, kupunguza msongamano darasani pamoja na utoro wa rejareja.

Mhe.Kikwete amezindua pia madarasa Sita yatakayotumika kwa kidato cha Tano na Sita katika shule ya sekondari Kanga. Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 150 utawezesha pia vijana kuishi bweni na kuboresha mazingira ya malazi na Ujifunzaji kwa wanafunzi.

Amezindua ujenzi wa barabara za Mkwajuni mjini kwa Kiwango cha lami wenye thamani ya shilingi milioni 760, Mhe. Kikwete amempongeza Mbunge wa jimbo la Songwe, Mhe. Philipo Mulugo kwa kuelekeza kiasi cha shilingi Milioni 500 za mfuko wa maendeleo ya Jimbo kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete amezindua Mradi wa usambazaji umeme Kitongoji cha Kikuyuni kata ya Mkwajuni wenye thamani ya shilingi milioni 156. Amesema, fedha hizo zimetolewa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kuchochea maendeleo na ustawi wa watanzania hususani waishio vijijini.

Mkuu wa mkoa wa Songwe, Mhe.Daniel Chongolo amemhakikishia Mhe.Waziri Kikwete kuendelea kutekeleza miradi kwa ufanisi ili kuweza kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi za wananchi wa mkoa huo. Vile vile Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Chongolo ametumia ziara hiyo pia kuwahimiza wananchi kulinda na kuyatetea maendeleo yao kwa wivu kwa kuwa hilo ndilo lengo la Serikali yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mara baada ya kuzindua miradi hiyo, wamemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kueleza kuridhishwa na kasi ya maendeleo.