Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali yaja na mwarobaini ucheleweshwaji michango ya Hifadhi ya Jamii


SERIKALI YAJA NA MWAROBAINI UCHELEWESHWAJI MICHANGO MIFUKO YA HIDADHI YA JAMII

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imewasilisha muswada wa marekebisho ya sheria za mifuko ili kuzipa nguvu bodi za wadhamini za mifuko kupunguza ama kusamehe tozo zinazotokana na ucheleweshaji wa michango.

Aidha, marekebisho hayo yatawezesha waajiri wenye malimbikizi kulipa madeni na kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati.

Mhe Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Juni 28, 2024 wakati akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa 15 wa Bunge jijini Dodoma.

Amesema kuwa katika kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati sheria za mifuko zinawataka waajiri kuwasilisha taarifa ya maandishi kwenye mifuko ndani ya miezi sita kabla ya mtumishi kustaafu ambapo mifuko inatakiwa ndani ya siku 60 baada ya mwananchama kustaafu awe analipwa mafao yake.

Kadhalika, Mhe. Majaliwa ametoa rai kwa waajiri nchini kuhakikisha wanalipa michango ya watumishi wao kwa wakati.

Pia ameiagiza mifuko kuchukua hatua kwa waajiri wanaokiuka wajibu wao wa kuwasilisha michango kwa wakati.

"Bodi na Menejimenti za mifuko tumieni vifungu vya Sheria kuhakikisha michango inawasilishwa kwa wakati ili kuwaondolea wastaafu changamoto za kulipwa mafao," amesema Mhe. Waziri Mkuu