News
Serikali inatambua mchango wa WCF katika kulinda nguvu kazi ya Taifa
Serikali inatambua mchango wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kulinda haki na ustawi wa wafanyakazi ambao ni nguvu kazi ya Taifa na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa WCF leo Februari 17 2025, mjini Morogoro.
Mhe. Katambi amesema kuwa kupitia WCF wafanyakazi wanaopata ajali au ugonjwa unaotokana na kazi zao wanapatiwa matibabu, fidia ya ulemavu, au pensheni kwa wale wanaopoteza uwezo wa kufanya kazi kabisa na hivyo kuwawezesha kuendelea na maisha yao bila kudhoofika kiuchumi.
“Jambo hili linaleta utulivu mahala pa kazi kwa kuliondoa jukumu la kulipa fidia kwa mwajiri hivyo kupunguza lawama na malalamiko”, amesema Mhe. Katambi.
Aidha Waziri Katambi amepongeza jitihada zinazofanywa na Menejimenti ya WCF ikiwemo kuweka misingi madhubuti katika usimamiaji wa sera, sheria, taratibu ya mifumo ya kifedha.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho cha siku mbili chini ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma, kitajadili na kupitisha Mpango wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.