News
Mhe. Ridhiwani Kikwete azindua baraza la LESCO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua Baraza la Ushauri wa masuala ya Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO) leo Machi 3, 2025 Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Baraza hilo, Mhe. Kikwete amewataka wajumbe wa baraza hilo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na uzoefu katika masuala ya Kazi, Ajira, Uchumi na Jamii huku wakitanguliza mbele maslahi ya nchi, uzalendo, uadilifu, haki na wajibu wa pande zote ili kukidhi falsafa ya serikali ya awamu ya sita ya katika kuhudumia wananchi.
“Ni matarajio yangu baraza litatekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kufanikisha azma ya serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga Uchumi, kukuza Ajira na kuhudumia jamii” amesema
Vile vile, amesisitiza baraza hilo kutoa maoni na ushauri kuhusu sera, sheria, mikakati, kanuni na miongozo itakayosaidia kukuza kazi za staha, kuendeleza na kujenga Uchumi, kuongeza tija na uzalishaji kwa ujumla.
Aidha, kwa mujibu wa Sheria za Kazi Kifungu (5) Sura 300, LESCO ina majukumu mengi inayoyatekeleza ikiwa ni Pamoja na kumshauri Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Kazi na Ajira kuhusu masuala yote yanayohusu Kazi, Ajira, Uchumi na Jamii.