News
Mhe. Ridhiwani azindua bodi ya wadhamini NSSF
✅Ameitaka Bodi kuhakikisha Mfuko unawafikia wananchi wengi waliojiajiri na kuwa elimisha umuhimu wa kinga ya Jamii
Na, Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amezindua Bodi mpya ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii [NSSF], ambapo ameitaka kuzingatia sheria, sera, kanuni, na miongozo mbalimbali inayotolewa na serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Uzinduzi huo umefanyika leo (Ijumaa Machi 14, 2025) Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga, Mkurugenzi wa Mfuko wa NSSF, Masha Mshomba na Menejimenti ya Mfuko huo.
Aidha, Mhe. Kikwete amesema Bodi hiyo ina wajibu wa kusimamia Mfuko huo kama ilivyoelekeza katika Sheria ya Mfuko wa NSSF kifungu cha 55 mpaka kifungu cha 57, hivyo ameitaka bodi hiyo kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mfuko unaozingatia uboreshaji wa huduma kwa wanachama, michango, uwekezaji na kulipa mafao.
Vile vile, Mhe. Waziri Kikwete amesema Serikali imeendelea kusimamia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa lengo la kuhakikisha wananchi wengi wananufaika na kinga ya jamii.
“Kampeni ya “NSSF Staa wa Mchezo” ni mpango kubwa unaolenga kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri kwenye sekta kilimo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji mdogo wa madini, waendesha bodaboda na mama/baba lishe ili waweze kunufaika na mafao ya muda mrefu na muda mfupi yakiwemo mafao ya matibabu,” amesema
Pia Mhe. Kikwete ameitaka bodi hiyo kusimamia vyema fedha za wanachama kwa kuzingatia miongozo inayotolewa Serikali pamoja na wataalamu wa sekta ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha mfuko unawekeza kwenye miradi yenye tija.
"Uwekezaji salama utafanya mfuko huu kuwa imara, endelevu na kuweza kulipa mafao stahiki kwa wanachama wake kwa wakati," amesema
Kwa upande wengine, amehamasisha menejimenti ya NSSF, kushirikiana vizuri na bodi hiyo mpya kuipitisha bodi hiyo kwenye miradi na programu mbalimbali wanazotekeleza ili waweze kutoa maoni na ushauri katika utekelezaji mzuri wa shughuli hizo.