News
Mhe. Katambi: Serikali kuendelea kujumuisha Wenye Ulemavu na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi
Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mikakati maalum ya kuwajumuisha Watu wenye Ulemavu kwenye Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini pamoja na Programu zingine ili kuwawezesha washiriki katika shughuli za kiuchumi na kujiletea maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Mhe. Patrobas Katambi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wasiyoona (Braille) yaliyofanyika leo Februari 21, 2025 Mkoani Tabora ambapo Vijana Wenye Ulemavu 471 wamenufaika na Programu hiyo.
Aidha, amesema serikali inatambua umuhimu wa vitabu vya nukta nundu kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wasioona kushiriki katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji na tayari vitabu hivyo vimesambazwa Shuleni na Vyuoni kuwasaidia wanafunzi katika masomo yao.
Katika hatua nyingine, Mhe. Katambi amesema Serikali imeendelea kuajiri Walimu wakiwemo Walimu wenye mahitaji maalumu ambapo kwa mwaka wa fedha2023/2024. zaidi ya walimu 10,000 wakiwemo Walimu wa Wanafunzi wenye mahitaji maalum wameajiriwa.
Hata hivyo, amewasisitiza Watu wenye Ulemavu kushiriki katika uchaguzi na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi wa kisiasa Kwa kuzingatia kauli mbiu ya maadhimisho ya Mwaka huu inayosema “Kupiga au kupigiwa kura ni haki kwa watu wasioona; Braille ni nyenzo kuu ya mawasiliano kwa ushiriki huru wakati wa uchaguzi”.