Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​Mhe. Katambi azindua Kongamano la Vijana Dodoma


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi leo tarehe 10 Agosti, 2024 amezindua Kongamano la vijana Jijini Dodoma ikiwa ni kuelekea siku ya vijana kimataifa Agosti 12, 2024.

Kongamano hilo ambalo linaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya Vijana linalofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete ambapo takribani vijana 3000 wamehudhuria.

Mhe. Katambi amesema asilimia 55.6 ya nguvu kazi ya taifa ni vijana na ndiyo kundi kubwa ambalo linategemewa sana katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo na ustawi katika taifa.

Aidha, amebainisha mikakati ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan namna ambayo imeendelea kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana ikiwemo kusimamia na kuratibu programu za kukuza Ujuzi ili kuwezesha nguvu kazi kumudu ushindani katika soko la ajira.

Vile vile, Mhe. Katambi amesema Serikali imeendelea kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana katika masuala ya ujasiriamali, uanzishaji wa miradi ya kiuchumi, urasimishaji, uendeshaji wa biashara pamoja na uongozi ili kuendesha shughuli zao kwa weledi.

Sambamba na hayo, amesema Serikali inaendelea kuwawesha vijana kupata maeneo ya kufanyia shughuli za uzalishaji mali kwa kuhamasisha halmashauri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya kufanyia shughuli za uzalishaji mali.

Awali akizungumza Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amehamasisha vijana kutumia vizuri kongamano hilo kujadili masuala mbalimbali yatakayokuza na kuimarisha ustawi wao.