Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Mhe. Katambi akagua maandalizi kilele cha mbio za Mwenge wa uhuru 2024


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amekagua maandalizi ya shughuli za kilele cha mbio za mwenge wa uhuru 2024 zitakazofanyika Oktoba 14, 2024 Jijini Mwanza.

Ziara hiyo imefanyika leo Septemba 23, 2024 Mkoani humo ambapo amekagua maendeleo ya vijana wa halaiki, uwanja wa CCM Kirumba yatakapofanyika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024; uwanja wa Furahisha itakapo fanyika wiki ya vijana na Kanisa la Nyakahoja Parokia ya Mtakatifu Fransisco Xavier (Jimbo kuu la Mwanza) itakapofanyika ibada ya maalumu ya kumuombea Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Aidha Mhe. Katambi amepongeza Mkoa wa Mwanza kwa namna ulivyojipanga kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki kwa wingi katika kilele cha mbio za mwenge wa uhuru.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema kuwa Mkoa huo umejipanga vyema na kuhitimisha Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2024.

Katika ziara hiyo, Mhe. Katambi ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mary Maganga, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana, Elikim Mtawa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Shaib Mohamed.

Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2024 zinaenda sanjari na kumbukizi ya matukio adhimu katika taifa letu ambayo ni Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Miaka 60 ya mbio za Mwenge wa Uhuru ambapo zilianza rasmi mwaka 1964. Pia mbio za Mwenge wa Uhuru zinaadhimisha kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha muasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.