Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Katambi “Serikali imetoa shilingi Bilioni 3 kwa vikundi vya Vijana”


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, amesema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikitenga shilingi Billion moja kila mwaka katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa ajili ya mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana ambapo hadi sasa, shilingi Billion 3.2 zimekwishatolewa.

Akiongea na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, kuhusiana na Kilele cha Siku ya Kimataifa ya Vijana Duniani terehe 12 Agosti, 2022, Mhe. Katambi amaebainisha kuwa Kupitia Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa na Ofisi hiyo fedha hizo zimekwishatolewa kwa vikundi vya vijana 586 vyenye wanachama 4,222 kwenye Halmashauri za Wilaya 155.

Kaulimbiu maalum kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa kwa mwaka huu ambayo huandaliwa na Umoja wa Mataifa ni; “Kila Mmoja Anahusika katika Kujenga Uchumi Imara, Ustawi na Maendeleo Endelevu: Jiandae Kuhesabiwa”.

Mhe. Katambi amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuweka mikakati endelevu ya kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali ili kuendeleza uchumi wa Taifa, kwa kuelekeza Halmashauri za Wilaya zote nchini kutenga asilimia nne ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwapatia vijana mitaji ya kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali ambapo Mikopo hiyo haitozwi riba.

Aidha, amesisitiza kuwa Halmashauri za Wilaya zote nchini zimeagizwa kutenga maeneo maalum ya shughuli za kiuchumi kwa vijana (Youth Economic zones) na zimesisitizwa kuhakikisha meneo hayo yanawekewa miundo mbinu na huduma muhimu kwa jamii.

Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha Programu ya Stadi za Maisha kwa Vijana walio Nje ya Shule kwa lengo la kuhakikisha kuwa vijana wanaweza kukabiliana na changamoto zitokanazo na shinikizo rika.

“Programu ya kukuza Ujuzi wa Nguvu Kazi ya Taifa ambayo asilimia 56 ni vijana imeanzishwa. Kupitia Programu hiyo, vijana 28,941 wamekwishapatiwa mafunzo ya Uanagenzi, Vijana 20,432 wametambuliwa na kurasimisha ujuzi wao uliopatikana nje ya Mfumo rasmi wa shule. Vile vile, vijana 5,975 wahitimu wa elimu ya juu wa fani mbalimbali wamewezeshwa kupata mafunzo ya uzoefu kazini”

Mhe. Katambi amefafanua kuwa Kupitia katika program hiyo, pia elimu ya kilimo kinachotumia teknolojia ya Kitalunyumba (Green house) imetolewa kwa vijana 8,980 katika Mikoa 12 yenye Halmashauri za Wilaya 84 katika awamu ya kwanza. Aidha, amebainisha kuwa Mikoa yote iliyobaki inatarajiwa kufikiwa na kufanya jumla ya vijana 18,700 watakaopatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa.