News
Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii yaridhishwa na Usalama, Afya Viwandani
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wameridhishwa na Usalama na Afya Mahali pa Kazi katika Kiwanda cha Elsewedy electricity na Kiwanda cha Knouf.
Akizungumza leo Novemba 12, 2024 Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Toufiq, amevipongeza viwanda hivyo kwa kukidhi mahitaji ya sheria ya Afya na usalama mahali pa kazi pamoja na kanuni zake.
Aidha, amesema kamati itaendelea kuishauri serikali kuendelea kulinda nguvu kazi ya wafanyakazi viwandani na maeneo yote ya kazini.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Riziki Lulida amepongeza viwanda hivyo kwa kuweka miundombinu rafiki kwa wenye ulemavu na kutoa wito kwa viwanda hivyo kuzingatia asilimia tatu ya Watu wenye Ulemavu kwenye ajira.
Awali akizungumza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete, amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao ambao wanazalisha na kusafirisha bidhaa nje ya nchi, hali inayo changia kukuza uchumi wa Taifa.
Sambamba na hayo, Mhe. Ridhiwani amepongeza kwa wawekezaji hao kutoa fursa kwa vijana kupata ajira katika viwanda hivyo.
Akihitimisha ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi Khadija Mwenda, amewasisitiza Waajiri nchini kuendelea kuzingatia sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.