Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Kamati ya Bunge yapongeza serikali awamu ya sita uwezeshaji Vijana kiuchumi


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imepongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongizwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwezeshaji vijana kiuchumi ili waweze kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Aidha, wamepongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa uratibu na usimamizi wenye tija katika kutoa Mikopo kwa Vijana kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Toufiq Machi 12, 2025 wakati wa ziara ya kamati hiyo Jijini Arusha iliyolenga kukagua Mradi wa Kilimo wa kikundi cha vijana cha Agri Genius Group.

Mhe. Toufiq amesema Mikopo hiyo imewasaidia Vijana kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za uzalishaji mali ili kujikwamua kiuchumi.

Vile vile, amempongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuwakwamua vijana kiuchumi ikiwemo kuridhia kutoa mikopo yenye riba nafuu.

Awali akizungumza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema kipindi cha cha mwaka 2009/2010 hadi Mwaka 2024/2025 jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 8.9 imetolewa kwa miradi ya vijana 1,126.

Naye, Mwenyekiti wa Kikundi cha Agri Genius Youth Group, Godfrey Rogath ameshukuru serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwawezesha mkopo wa shilingi Milioni 30 ambayo imewezesha kikundi hicho kuzalisha kwa tija na kutoa fursa za ajira kwa vijana wengine.