Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Waziri Ndejembi awataka Waajiri kusajiri maeneo ya kazi OSHA


* Ahimiza waajiri kuendelea kutekeleza Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka wamiliki wa maeneo ya kazi kuhakikisha wanasajili maeneo yao ya kazi OSHA sambamba na kutekeleza sheria ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuboresha mazingira ya kazi nchini.

Mhe. Ndejembi ametoa agizo hilo hii leo Aprili 23, 2024 wakati akizungumza na waandishi kuelekea Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani ambayo uadhimishwa tarehe 28 Aprili kila Mwaka.

Aidha, Waziri Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa kulinda nguvukazi ya taifa kwa kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magojwa yatokanayo na kazi.

Vile vile, Mhe. Ndejembi ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) kuendelea kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi kupitia programu ya “Afya Yako Mtaji Wako” ambayo inaratibiwa na ofisi hiyo, ili kukuza uelewa wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema kuelekea maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi, serikali kwa kushirikiana na wadau wa utatu inaendesha kampeni maalum ya uhamasishaji kwa kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa makundi mbalimbali.

Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani 2024 yatafanyika katika viwanja vya General Tyre, jijini Arusha yakiongozwa na kauli mbiu isemayo: “Athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi katika Usalama na Afya Kazini; Sajili eneo la kazi OSHA katika harakati za kupunguza athari hizo”.