Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

​WANANCHI WAHAMASISHWA KUSHIRIKI KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) amehimiza wananchi wa Mkoa wa Tanga kushiriki kwa wingi katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.

Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa Mkwakwani Waziri Mhagama alisema kuwa Mkoa wa Tanga umepewa heshima kuwa wenyeji wa Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa yatakayofanyika Oktoba 14, 2018 katika uwanja wa Mkwakwani mkoani Tanga.

Mhe. Mhagama ameeleza kuwa Mgeni Rasmi anatarijiwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein ataungana pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na Viongozi mbalimbali ambao pia watashiriki Ibada ya kumbukumbu ya baba wa taifa Mwl. Julius K. Nyerere, itakayofanyika siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba, 2018 katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Anton, Mjini Tanga.

“Mwenge wa Uhuru ni tunu ya taifa na unawakupusha wananchi hususan vijana historia ya Baba wa Taifa juu ya mambo mengi aliyoyafanya katika kudumisha Muungano na umoja wa Taifa letu” alisema Waziri Mhagama

Aliongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu itakabidhi rasmi mpango mkakati wake kwenye maadhimisho hayo unaolenga kutoa ujuzi kwa vijana nchini ili waweze kujiajiri kwenye sekta ya kilimo kwa kutumia ujuzi na utaalamu mpya wa kilimo cha kitalu nyumba.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigela amesema kuwa sherehe hizi ni za kihistoria na hivyo aliwasihi wakazi wa Tanga kushiriki kwa wingi ili waweze kusikiliza yanayotarajiwa kuzungumzwa na viongozi watakaokuwepo kwenye maadhimisho hayo.

Kauli Mbio ya Mwenge wa Uhuru 2018 ni “Elimu ni ufunguo wa maisha wekeza sasa kwa maendeleo ya taifa letu”