Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

VIJANA 3,440 WANUFAIKA NA PROGRAMU YA UKUZAJI UJUZI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Mbunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) amewaasa vijana 3,440 waliomaliza mafunzo ya ufundi kupitia programu ya ukuzaji ujuzi nchini inayotekelezwa na Serikali kutumia mafunzo hayo kujiajiri.

Akizungumza leo wakati wa mahafali ya vijana waliohitimu mafuzo hayo katika vituo vya Don Bosco Net Tanzania Mhe. Mhagama amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kukuza ujuzi kwa vijana ili kuchochea maendeleo na ujenzi wa uchumi wa viwanda.

“Kazi ya kuwaandaa vijana kielimu na kiujuzi inayotekelezwa na Serikali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka ya 2015 kupitia ibara ya 59 na 60 zinazoelekeza Serikali kuwaandaa vijana kielimu kiujuzi ili waweze kushiriki katika kujiletea maendeleo” Alisisitiza Mhe. Mhagama

Mafunzo ya ufundi kupitia programu ya kukuza ujuzi yalijikita katika fani za magari, ushonaji nguo, ujenzi wa nyumba, uchongaji vipuri,TEHAMA, Useremala ambapo mafunzo hayo yanafadhiliwa na Serikali ya Tanzania.

AkifafanuaMhe. Mhagama amesema kuwa programu ya kuwajengea uwezo vijana kwa kukuza ujuzi wao ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa wakati akihutubia Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa tuwapatie vijana ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Takribani wanagenzi zaidi ya 3000 wamehitimu mafunzo ya kukuza ujuzi kwa vijana yalifonyika ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuwawezesha vijana kujiajiri.

Katika kutekeleza azma hii Serikali imeelekeza juhudi za kuwawezesha vijana kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo ya Kilimo kupitia mpango wa Maendeleo ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) kwa kuwa sekta ya kilimo inaajiri asilimia 66.3 ya ajira zote nchini.

Pia alizikumbusha Halmashuri zote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Vijana ikiwa ni pamoja na kilimo, Pia aliwahimiza wanawake kushiriki kwa wingi kwenye mafunzo haya yatakapo anzishwa tena ili wakapate taaluma itakayowasaidia kuwawezesha kimaisha.

Alizitaka Halmashauri pia kutenga asilimia 4 ya mapato yake kwa ajili ya kuwawezesha vijana na akina mama ili waweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi na ustawi wao.

Naye Mkuu wa Shirika la Don Bosco Kanda ya Afrika MasharikiPadre. Saimon Asira amesema kuwa anawapongeza wakufunzi walioshiriki katika kuwaandaa vijana hao kwa kuwa wametekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa.

“Ninawaomba vijana waliopata mafunzohaya kutumia ujuzi waliopata kupitia programu hii na wakawe chachu kwa vijana wengine kwa kufanya kazi kwa biddii na maarifa” Alisisitiza Padre Asira

Kwa upande wake mkurugenzi wa Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Ally Msaki amesema dhamira ya Serikali ni kuondoa tatizo la ajira kwa vijana kwa kuwajengea uwezo wa kujiajiri ili waondokane na changamoto ya umasikini.

“Mafunzo haya yameweza kuwajengea uwezo Vijana ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwakwamua vijana kiuchumi ili waweze kushiriki katika shughuli mbalimbali.” Alisema Msaki.

Nae mmoja wa wahitimu Bi. Selestina Katwazo aliweza kuishukuru Serikali kwa kuwafanikishia kuweza kupata mafunzo haya ambayo yamewabadilisha kimaisha na kuwajengea uwezo wa kujiamini katika kufanya shughuli za kimaendeleo.