Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ipo mbioni kurekebishwa - Ndejembi


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Mhe. Deogratius Ndejembi amewahakikishia Majaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na wadau wengine kuwa, Serikali inayachukulia kwa uzito mkubwa maoni yao kuhusu kuboresha baadhi ya vifungu vya sheria ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

Mhe. Ndejembi ameyasema hayo wakati wa kufunga kikao kazi kati ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania - Divisheni ya Kazi, Kanda ya Kati ya Magharibi, Kamishna wa Kazi, Menejimenti ya Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Aprili 20, 2024 Mkoani Kigoma.

“Tayari maoni mliyotoa ya kuboresha kifungu cha 39 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kilichoweka ukomo wa muda wa kuwasilisha madai bila kutoa wigo wa kupokea madai hayo iwapo kuna sababu za msingi za kucheleweshwa kwake, tumeshayafanyia kazi na maboresho hayo kuwa sehemu ya muswada wa marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii uliosomwa Bungeni kwa mara ya kwanza tarehe 15 Februari 2024.” Amesema Mhe Ndejembi.

Aidha Mhe, Ndejembi amesema WCF kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Hifadhi ya Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), wanaendelea na uchambuzi wa maboresho ya sheria ya fidia kwa wafanyakazi ambayo yalitolewa na Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.