Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI YAENDELEA NA MKAKATI WA KURASIMISHA AJIRA ZA SEKTA ISIYO RASMI NCHINI


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu (Idara ya Ajira) kwa kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali wameendelea na mkakati wa kupanga namna bora ya kurasimisha ajira za sekta isiyo rasmi nchini.

Hatua hii ni katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ambayo imeweka kipaumbele katika kuhakikisha inaondoa umasikini kwa kuwawezesha watu walio katika sekta isiyo rasmi kuwa na ajira au shughuli zenye tija kwa manufaa yao na manufaa ya nchi kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Mkurugenzi wa Ajira Bw. Ally Msaki alisema kuwa majadiliano haya yatachangia katika kuwatambua wajasiriamali pamoja na wafanyabiashara wadogo kwa kubaini mahitaji yao na kuwawezesha kushiriki na kuchangia katika uchumi wa taifa letu.

“Urasimishaji huu utasaidia kutambua vikundi mbalimbali vya wajasiriamali na wafanyabashara wadogo kwa kuzifanya shughuli zao kuwa zenye manufaa makubwa na endelevu” alisema Msaki.

Aidha aliongeza pia, sehemu kubwa ya nguvu kazi ya taifa letu ni vijana, hivyo urasimishaji wa shughuli zao kutawawezesha kutambulika, kupata mitaji yenye masharti nafuu vilevile urahisi wa kuwapatia mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi katika kuboresha shughuli zao.

Kwa upande wake Bi. Rehema Shao kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alieleza kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishaanza kusajili wajasiriamali wa sekta isiyo rasmi kwa kuwapatia TIN na hivi karibuni tumeanza kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara wadogo ili kuweza kuwatambua pamoja na shughuli wazifanyazo.

“Ushirikiano wa wadau katika zoezi hili ni wa muhimu na ni njia bora itakayopelekea matokeo chanya kwa kupunguza kiwango cha umasikini pamoja na kuongeza walipa kodi kwa kuwawezesha wahusika kuwa na kazi za staha” alisema Shao

Mkutano huo umekutanisha wadau kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, MKURABITA, NSSF, TRA, TBS, TFDA, SSRA, CISO (T) na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

MWISHO