Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI KULETA MABADILIKO YA KIUCHUMI KWA WAFANYAKAZI NCHINI
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) alipokuwa akiongea na viongozi wanawake wa Mkoa wa Morogoro kutoka vyama vya wafanyakazi ikiwemo TAMIKO, CWT, TUICO, TALGU, TULGE, TPAWU na CHODAWU.

Waziri Mhagama amebainisha kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imelenga kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wafanyakazi kwa kuhakikisha wanashirikishwa kwenye dhana ya uchumi wa viwanda. Lengo likiwa ni kuwawezesha wafanyakazi wanashiriki katika mipango ya maendeleo ya taifa kwa kufuata kanuni na taratibu ya dhana nzima ya uchumi wa viwanda.

"Mnao uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na mkawa chachu ya maendeleo ya viwanda kwenye uchumi wa taifa letu, kwa kuweza kutoa ajira, vilevile kuwasaidia ninyi kupiga hatua za maendeleo kwa kufanya kazi kwa uzalendo na weledi kwa kutumia sera ya viwanda" ameeleza Waziri Mhagama.

Aidha, aliongeza kuwa, Sera ya uchumi wa viwanda iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ni jambo jema linalolenga kuboresha maisha ya watanzania.

“Mheshimiwa Rais amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza azma ya kujenga Tanzania ya viwanda, hivyo nitafurahi sana kama Waziri mwenye dhamana ya wafanyakazi kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa wafanyakazi.” Alisema Mhagama.

Alitoa rai kwa viongozi wanawake kuhakikisha wanaratibu na kusambaza ujumbe huu wenye habari njema kwa wanawake nchi nzima waliopo kwenye sekta ya ajira kuchangamkia fursa hii kwa kuanzisha miradi mbalimbali itakayowawezesha kuwakomboa kiuchumi.

Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa alifafanua juu ya sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo imelenga kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji ili kuwawezesha wananchi.

“Wanawake wanamchango mkubwa katika jamii, hivyo ni vyema mkatumia vizuri fursa hii kwa kuanzisha shughuli zitakazo wasaidia kuongeza vyanzo vya mapato na kuleta maendeleo kupitia ushirika wenu na hivyo kuwarahisishia kupata mikopo ya kuendeleza shughuli hizo.” Alisema Bi. Issa

Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhoke aliungamkono rai iliyotolewa na Waziri kwa kuhaidi suala hili watalifikisha na kulifanyia kazi kwenye shirikisho la vyama vya wafanyakazi.

Mmoja wa washiriki kutoka (TALGU) Bi. Elizabeth Ngaiza aliishukuru Serikali kwa kuwapatia fursa hii wafanyakazi kuweza kuanzisha shughuli za kimaendeleo zitakazowaongezea kipato ambacho kitawasaidia kuendesha majukumu ya kifamilia tofauti na hapo awali walikuwa wakitegemea mshahara ambao ulikuwa hautoshi kutekeeza baadhi ya majukumu.

Katika mkutano huo Waziri Mhagama aliambatana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na wawakilishi kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Benki ya NMB na SIDO ambao waliweza kuelezea fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotolewa katika mashirika hayo.