Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

Serikali kuendeleza ushirikiano na ILO katika programu za ajira kwa vijana


Serikali kuendeleza ushirikiano na Shirika la Kazi Duniani (ILO) katika programu na mipango mbalimbali hususan kwenye masuala ya kazi nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameyasema hayo alipokutana na kufanyamajadiliano na wajumbe wa shirika hilo na watendaji wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Ofisi yake walipokutana hii leo Oktoba 27, 2018 Bungeni Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa mkutano huo Waziri Mhagama alisema kuwa zipo programu ambazo zinafanyiwa kazi na ILO kwa kushirikiana na Serikali kwenye masuala ya maendeleo ya ajira kwa vijana, ikiwemo kuwajengea ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri au kuunganishwa kwenye masoko ya ajira ambayo tunayo hapa nchini.

“Programu hizi zitakuwa ni chachu katika kutatua masuala mbalimbali na kuleta maendeleo ambayo yatafanikisha mipango ya serikali,” alisema Mhagama.

Aidha, aliongeza kuwa programu hizo zitawajumuisha vilevile watu wenye ulemavu kwa kuwapatia mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kupitia programu hizo.

Katika hatua nyingine kikao hiko kimekubaliana kuanzisha kamati ya pamoja ambayo itaangalia programu za ILO namna ambavyo zinaweza kuuwiana na programu za Serikali.

Mhe. Mhagama alilishukuru shirika hilo kwa mchango wake katika kusaidia masuala mbali mbali ikiwemo programu ya Taifa ya Kazi za Staha, ukuzaji ujuzi, programu ya kuhamasisha uwekezaji wenye kuzalisha fursa za ajira, mapitio ya sera za kinga ya jamii na ajira, uridhiaji wa mikataba ya viwango vya kazi vya kimataifa, maandalizi ya mkakati wa kutokomeza ajira mbaya kwa watoto na mkakati wa kutokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi maeneo ya kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Wallington Chibebe alisema kuwa ILO itaendeleza programu hizo kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali ambazo ni pamoja na kuendeleza mafunzo ya kazi za uanagenzi zitawawezesha vijana kujiajiri.

“Ushirikiano ndio jambo muhimu katika kutekeleza majukumu tuliopanga kwa faida ya kuimarisha maendeleo ya jamii kwa ujumla,” alisema Chibebe.