Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WATU WENYE ULEMAVU NCHINI


Serikali kupitia Kitengo cha Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu imedhamiria kuendelea kutatua changamoto za watu wenye ulemavu nchini kwa kuhakikisha inaratibu kikamilifu masuala ya watu wenye ulemavu.

Hayo yameelezwa hii leo (Septemba 09, 2018) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa Warsha ya siku moja ya masuala ya watu wenye ulemavu kwa Waheshimiwa Wabunge Jijini Dodoma.

Waziri Mhagama alisema kuwa masuala ya watu wenye ulemavu ni la kimtambuka hivyo ni vyema tukathamini kundi hili katika kutatua changamoto wanazokumbana nazo.

“Sisi kama Serikali tutendelea kuratibu na kuhakikisha tunatatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutekeleza Sheria na kanuni zinazowalinda na kuelekeza namna ya kuwahudumia watu wenye mahitaji maalum,”alisema Waziri Mhagama.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) Bi. Ummy Nderiananga alieleza kuwa, uwepo wa Idara ya Wenye ulemavu katika Ofisi ya Waziri Mkuu ni sehemu ya mafanikio makubwa kwaniimeleta chachu katika utatuzi wa baadhi ya mitazamo hasi ikiwemo ule wa kuona kundi hili ni la kusaidiwa na lisilojiweza.

“Kimsingi niishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu na kushughuliki masuala ya Watu wenye Ulemavu kama kundi maalum kwani awali tulikuwa wanyonge na kuona wenye kuhitaji misaada, wakati ni watu wenye uwezo wa kujitegemea na kuchangi vyema katika maendeleo ya Nchi yetu” alisema Bi. Nderiananga.

Kwa upande wake Mbunge wa Malindi Mhe.Ally Saleh aliipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwao na kushauri kuwa na takwimu halisi ya watu wenye ulemavu nchini ili kuweza kuwafikia katika kuwahudumia watu wenye ulemavu.

“Kipekee naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendelea kuratibu masuala ya watu wenye ulemavu ingawa ushauri wangu ni kuwa na mikakati inayotekelezeka kwa kuwa na takwimu za watu wenye ulemavu nchini ili kuweza kufuatilia changamoto zao na kuzitatua,” alisisitiza Mhe.Saleh

Aidha Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wenye Ulemavu Bw. Jacob Mwinula alisisitiza juu ya kuendelea kutekeleza sheria ya Watu wenye ulemavu Na.9 ya Mwaka 2010 inayoeleza utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ambayo imekuwa ikielekeza katika utoaji wa huduma za afya, misaada kijamii, huduma za msingi ikiwemo elimu na mafunzo stadi na mawasiliano.

AWALI

Warsha hii ya siku moja imelenga kujenga uelewa kwa Waheshimiwa Wabunge juu ya masuala ya Watu Wenye Ulemavu, Kushauri juu ya namna bora ya kuwahudumia wenye ulemavu pamoja na kutambua fursa zilizopo na Mipango iliyopo katika kushughuliki changamoto zinazowakali.

MWISHO