Tume ya Usuruhishi na Uamuzi

TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI (CMA)

Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ni miongoni mwa Taasisi sita zilizoundwa chini ya Sheria ya Taasisi za Kazi, Na. 7 ya Mwaka 2004. Tume hii imepewa jukumu la kusuluhisha na kutatua migogoro ya kikazi baina ya waajiri na wafanyakazi chini ya Kifungu cha 14 (1) cha Sheria ya Taasisi za Kazi, Na. 7 pamoja na Sheria Na. 6 za Mwaka 2004. Tume inatoa huduma zake katika mikoa yote ya Tanzania Bara.

Kiutendaji, ofisi za Tume zimegawanywa katika kanda kumi na moja (11) zifuatazo:

Kanda ya Dar es salaam inahudumia Makao Makuu, Temeke na Pwani, kanda ya Tanga inahudumia Tanga, Muheza, Lushoto na Korogwe, kanda ya Mtwara inahudumia Mtwara na Lindi, kanda ya Dodoma inahudumia Dodoma na Singida, kanda ya Iringa inahudumia Iringa, Mufindi na Njombe, kanda ya Ruvuma inahudumia Ruvuma pekee, kanda ya Tabora inahudumia Tabora na Kigoma, kanda ya Mbeya inahudumia Mbeya na Rukwa, kanda ya Mwanza inahudumia Mwanza, Shinyanga, Bukoba na Musoma, kanda ya Arusha inahudumia Arusha, Moshi na Manyara na kanda ya Morogoro inahudumia Morogoro na Kilosa.

Majukumu ya Tume

  • Kupokea na kuratibu migogoro yote ya kikazi inayowasilishwa kwenye Tume isipokuwa inayohusu Majeshi ya Ulinzi na Usalama
  • Kusuluhisha na kuamua migogoro yote inayowasilishwa kwenye Tume kwa mujibu wa Sheria za Kazi nchini
  • Kuelimisha na kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu ushirikishwaji wafanyakazi, taratibu za utatuzi na uzuiaji wa migogoro ya kikazi kwa waajiri na wafanyakazi pale ambapo ikiombwa kufanya hivyo
  • Kusimamia uundwaji wa Mabaraza ya wafanyakazi katika maeneo ya kazi