Idara ya Kazi

Idara ya Usimamizi Kazi na Huduma za Ukaguzi ambayo hapo awali ilijulikana kama Idara ya Kazi ina jukumu na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sheria za kazi na mahusiano bora sehemu za Kazi.

Idara hii imeundwa upya kutokana na mabadiliko katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi, Na. 7 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Na. 6 za Mwaka 2004.

Idara hii inaongozwa na Kamishna wa Kazi akisaidiwa na Makamishna wa Kazi Wasaidizi Watatu wanaoongoza Sehemu zifuatazo:-

· Mahusiano Kazini (Labour Relations)

· Ukaguzi Sehemu za Kazi (Labour Inspections)

· Hifadhi ya Jamii (Social Security)


1.Sehemu ya Mahusiano Kazini (Labour Relations Section)
  • Kuratibu na kusimamia mapambano dhidi ya Ajira ya watoto kwa kushirikiana na wadau nchini
  • Kuratibu na kusimamia mapambano dhidi ya maambukizi ya Ukimwi mahali pa kazi
  • Kuratibu na kuhamasisha uzingatiwaji wa masuala ya jinsia na kuhakikisha fursa sawa kwa wanawake na wanaume katika maeneo ya kazi
  • Kuratibu na kusimamia uendeshaji wa shughuli za baadhi ya Taasisi zilizoundwa chini ya sheria ya Taasisi za Kazi, Na. 7 ya 2004 ambazo ni Bodi za Mishahara za Kisekta (Sector Wage Boards) na Baraza la Ushauri kuhusu masuala ya Kazi, Uchumi na Jamii (Labour Economic and Social Council-LESCO).
2.Sehemu ya Ukaguzi Sehemu za Kazi (Labour Inspections Section)
  • Kuzuia migomo na migogoro ya kikazi kwa kufanya kaguzi na uelimishaji katika maeneo mbalimbali ya kazi kwa lengo la kuhakikisha Sheria za Kazi zinatekelezwa ipasavyo miongoni mwa Waajiri na Wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na kuandaa mchakato wa kuwafikisha Mahakamani wale wote wanaokiuka au kushindwa kutekeleza Sheria za Kazi na Kanuni zake
  • Kupokea nakala za mikataba ya makubaliano ya pamoja kuhusu hali bora za kazi kwa mujibu wa kifungu cha 71(7) cha Sheria Na. 6 ya 2004, iliyofikiwa baina ya Waajiri na Wafanyakazi kupitia Vyama vyao.
  • Kukuza majadiliano ya pamoja (Collective Bargaining) miongoni mwa wadau katika maeneo ya kazi
3.Sehemu ya Hifadhi ya Jamii (Social Security Section)
  • Kuendelea kupokea taarifa za ajali kazini, kushughulikia na kusimamia malipo ya fidia za ajali kwa Watumishi wanaoumia au kufariki kwa ajali Kazini kama inavyoelekezwa katika Sheria ya Fidia, Sura 263, R. E.2002 hadi hapo Sheria ya Fidia (Workers Compensation Act), Na. 20 ya mwaka 2008 itakapoanza kutumika
  • Kusimamia Sera, Sheria na utekelezaji wa Mpango wa Hifadhi ya Jamii nchini