Historia

IJUE WIZARA YA KAZI NA AJIRA

Wizara ya Kazi na Ajira, ni Wizara  inayowajibika na utoaji  wa huduma wenye lengo la kukuza ajira, usimamizi wa masuala ya sheria na Mahusiano Kazi, pamoja na kuratibu shughuli za usajili wa vyama vya Wafanyakazi na Waajiri.

Wizara inajihusisha pia na ushughulikiaji wa masuala mtambuka, kama vile kupambana na maambukizi ya ukimwi na kuhamasisha uzingatiwaji wa masuala ya jinsia.

Mamlaka ya utekelezaji wa shughuli za Wizara yanazingatiwa kwa misingi ya utatu, ambapo wadau mbalimbali kutoka makundi ya Waajiri, Wafanyakazi na Serikali hushirikiana kwa pamoja katika hatua mbalimbali za mipango na utekelezaji wa programu zilizo chini ya Idara na Taasisi za Wizara. Makundi mengineyo yanayoshirikishwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yanajumuisha Wabia Jamii wengine (kama vile Asasi Zisizo za Kiserikali (AZAKI), Taasisi Binafsi, n.k.) na Wabia Maendeleo (Kama vile Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO) na Mashirika mengine ya Kimataifa, Nchi Wahisani, n.k).

Historia ya Wizara

Wizara hii ni moja ya Wizara kongwe katika muundo wa Serikali tangu Uhuru mwaka 1961. Jina na muundo wake vimekuwa vikibadilika. Baada ya Uhuru Serikali iliunda Wizara mbali mbali ambapo mojawapo ni Wizara hii ya Kazi.         Mwaka 1961 hadi mwaka 1972 Wizara hii ilikuwa ikiitwa Wizara ya Kazi, Mawasiliano na Ujenzi.

Kati ya mwaka 1972 na 1984 ilibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi na Ustawi wa jamii. Kuanzia mwaka 1984 hadi 1987 ilibadilishwa tena na kuitwa Wizara ya Kazi na Utumishi. Mnamo mwaka 1987 muundo wa Wizara ulibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo.

Mwaka 1990 hadi 2000 jina lilibadilishwa na kuitwa Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana. Hata hivyo mwaka 2000 muundo  wake ulibadilishwa tena na kuitwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya  Vijana na Michezo hadi ilipofika mwaka 2005 ambapo muundo huo ulibadilishwa  na kuitwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, mwaka 2010 jina lilibadilishwa tena na kuitwa Wizara ya Kazi na Ajira baada ya kuondolewa Idara ya Maendeleo ya Vijana.

MUUNDO WA WIZARA

Ili kufanya kazi kwa ufanisi na kutimiza malengo yake, Wizara ya Kazi na Ajira ina Idara nne, ambazo ni Idara ya Usimamizi Kazi na Huduma za Ukaguzi, Idara ya Huduma za Ajira, Idara ya Utawala na Utumishi na Idara ya Sera na Mipango. Aidha Wizara ina vitengo vya Fedha na Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani, Msajili wa Vyama Huru vya Wafanyakazi na Waajiri, Habari, Elimu na Mawasiliano na Kitengo cha Ununuzi na Ugavi.

Vilevile Wizara inasimamia shughuli za mashirika na taasisi zifuatazo:-

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Tija la Taifa (NIP), Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya jamii (SSRA).