Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA AWATAKA VIJANA KUENZI MCHANGO WA BABA WA TAIFA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewataka vijana nchini kuenzi na kuziishi fikra na mitazamo za Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuendeleza umoja uliopo nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika Mkoani Lindi Oktoba 13, 2019, Waziri Mhagama alisema kuwa vijana wanapaswa kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake ili waendelee kujivunia juu ya misingi ya amani na umoja iliyopo nchini.

“Vijana mna kila sababu ya kujivunia amani na umoja ulipo katika taifa letu kwa kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi aliyewapenda watu wote bila kujali imani zao wala itikadi zao, alikuwa mzalendo na alitaka watanzania wote waishi kwa umoja,” alisema Mhagama.

Aidha alifafanua kuwa, Amani na umoja zilikuwa ni miongoni mwa tunu na falsafa kuu za Baba wa Taifa ambayo ndiyo matokeo ya umoja na mshikamano wa taifa uliopo sasa.

Aliongeza kuwa miongoni mwa mambo muhimu ambayo Baba wa Taifa alikuwa akisisitiza katika kuwaunganisha watanzania ni pamoja na kulijengea uhuru taifa na watu watu wake, kudumisha amani, upendo, umoja, uzalendo, mshikamano na kuandaa sera za kukabiliana na ujinga, umaskini na maradhi.

Pamoja na hayo alisisitiza pia vijana na wananchi kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuendeleza maono ya Baba wa Taifa ikiwemo mageuzi ya kiuchumi yenye manufaa kwa taifa.

Akitolea mfano sekta ya elimu ambayo serikali ya awamu ya tano imekuwa ikitoa elimu bure ilikuwa ni falsafa ya Mwalimu katika kuwajenga watanzania fikra ya kujitegemea ili waweze kuukabili umasikini.

Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo pia kuwahimiza wananchi kuendeleza maudhui ya Mwenge wa uhuru ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha watanzania na kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii ili wajiletee maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi alisema kuwa Mwalimu Julius Nyerere ataendelea kukumbukwa na Watanzania kwa mchango wake aliojitolea katika kulijenga taifa.