Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

WAZIRI MHAGAMA APONGEZA WAKULIMA WILAYA SAME KWA KILIMO CHA TANGAWIZI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amewapongeza wakulima wa zao la tangawizi na kukemea kilimo cha Mirungi Wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro.

Ametoa pongezi hizo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata tangawizi cha Mamba Miamba kilichopo katika Kata ya Myamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Januari 7, 2021.

Waziri alifurahishwa na wakulima hao kuwekeza katika kilimo cha tangawizi na kueleza kuwa, ni wakati muafaka kuachana na kilimo cha mirungi kwani Wilaya hiyo imekuwa ikijihusisha na kilimo hicho kwa muda mrefu.

“Wakulima shikamaneni na hakikisheni kilimo cha tangawizi kinakuna na tija na kuachana kabisa na kile cha mirungi, maeneo yenu yana rutuba ya kutosha kwa kilimo yatumieni kuzalisha kwa wingi tangawizi mjikwamue kiuchumi,”alisema waziri Mhagama

Aliongezea kuwa, katika maeneo yaliyokuwa yakimpa shida kwenye mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya mirungi ni pamoja na wilaya hiyo.

“Faraja ninayoipata leo ni kuona zao la tangawizi sasa linakwenda kuchukua nafasi ya kilimo cha mirungi na niwaombe Kamati ya Ulinzi na Usalama tujitahidi kuhakikisha tunatokomeza ulimaji wa mirungi kwa gharama yoyote”alisisitiza

Mpaka sasa Taifa limefanikiwa kukomesha matumizi na uingizaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90 kwa kuzingatia hatua mbalimbali ambazo zilichukuliwa na Serikali.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Anne Malechela alieleza furaha yake kwa ujio wa Waziri kujionea maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho huku akiahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa mkoa na wananchi kuhakikisha kiwanda kinakuwa na maendeleo endelevu ili kuleta matokeo chanya kwa wakazi wa Same na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa umma (PSSSF) Bw. Hosea Kashimba alieleza, namna walivyodhamiria kuwekeza katika kiwanda hicho na kuhakikisha kinaendelea kwa miaka mingi na kuleta tija.

“Katika kiwanda hiki tumewekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 kwa kuweka mtaji, na kufanya ukarabati wa majengo, kujenga uzio unaozunguka kiwanda pamoja na mifumo ya umeme kurahisisha shughuli za uendeshaji wake,”alieleza Kashimba

Aliongezea kuwa, hadi desemba 2020 mfuko umetoa shilingi Bilioni 1.3 za Kitanzania zilizotumika kununua mitambo ya kisasa, kufunga mifumo ya umeme kutoka TANESCO, Ukarabati wa jengo na kufunga mashine ambapo hatua hiyo imefikia asilimia 85.

Sambamba na hilo alieleza kuwa, kiwanda kitasindika tangawizi hadi tani 10 kwa siku na kusambaza bidhaa zake katika soko la ndani na nje ya nchi ambapo kitauza unga wa tangawizi katika nchi za Kenya, Uganda , Malawi, Afika Kusini, Uholanzi na nchi za Bara la Asia.

Mkurugenzi alibainisha zaidi ya ajira 40 zinatarajiwa kuzalishwa pindi uzalishaji wa kiwanda utakapoanza ambapo itaongeza tija kwa vijana na kutoa wito kuichangamkia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho.