News
Waajiri watakiwa kutoa mafunzo kwa Wafanyakazi
Serikali imetoa wito kwa waajiri nchini kuweka utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kuwa na uelewa wa pamoja ili kuepusha migogoro sehemu za kazi.
Wito huo umetolewa na Naibu Karibu Mkuu Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu,Kazi, Ajira,Vijana na Wenye Ulemavu Zuhura Yunus wakati wa ufunguzi wa semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi jijini Arusha (15 Septemba 2025) ambapo alisema watumishi na Waajiri wakielewa vyema Taratibu, Miongozo, Sheria na Kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma na masuala ya ajira na mahusiano kazini haitakuwa rahisi kuzikiuka.
Zuhura aliongeza kusema ni ukweli usiopingika kuwa, katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania masuala mengi yanayohusu mishahara na maslahi ya wafanyakazi yamepewa kipaumbele.
"Nimefurahi kuona kuwa, TUGHE mmeyaeleza kwa ufasaha masuala kadha wa kadha yanayowahusu Watumishi ambayo Serikali yetu imeweza kuyapatia ufumbuzi" alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Awali Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda alieleza kuwa idadi ya washiriki wa semina imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka huu TUGHE inatarajia kutoa mafunzo kwa washiriki zaidi ya 800 kutoka katika Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali, Bunge, Mahakama, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Afya za Serikali na zile za binafsi.
Mkunda alibainisha kuwa mafunzo haya yalianza kutolewa rasmi mwaka 2018 ambapo na yanakusudia kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa Waajiri na watumishi na wanachama wa TUGHE.