Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO SEKTA YA USAFIRISHAJI: WAZIRI MHAGAMA


Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya usafirishaji hapa nchini ili iweze kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi.

Akizungumza Novemba 1, 2019 Jijini Dodoma wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Vyama vya Madereva na Vyama vya Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji, Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kujenga mazingira wezeshi kati ya wadau wote wa sekta ya usafirishaji hapa nchini wakiwemo madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji.

“Moja ya maazimio ya mkutano wetu wa leo ni kuwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao hawajatoa mikata ya ajira kwa madereva wao waanze kutoa mikataba ya ajira iliyoboreshwa suala hilo lianze kutekelezwa mara moja kwa kuwa ni takwa la kisheria na sio jambo la hiari” Alisisitiza Mhagama

Kutolewa kwa mikataba hiyo ni matokeo ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mwaka 2017 yakitaka kuwepo kwa mikataba ya ajira iliyoboreshwa kwa madereva wote itakayoleta ustawi wa maslahi ya pande hizo na Taifa kwa ujumla.

Alifafanua kuwa mkutano huo umefanikisha kufikiwa kwa maazimio ya pamoja kati ya Serikali, wamiliki na madereva kupitia viongozi wa makundi hayo ili kuchochea ustawi wa sekta hiyo na kuondoa hali ya malalamiko na mapungufu yaliyobainika katika ukaguzi uliofanyika mwezi Julai na Agosti 2019 kwa lengo la kuona namna sheria za kazi zinavyozingatiwa.

Azimio jingine ni kuendelea kutoa elimu kwa makundi hayo kupitia vyama vya wamiliki na madereva ili kupunguza au kuondoa changamoto zilizopo hasa zilizoibuliwa katika ukaguzi uliofanyika hivi karibuni.

Aidha, Waziri Mhagama ameviagiza vyama vya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kuhakikisha wanaruhusu wafanyakazi kuanzisha matawi ya vyama vya wafanyakazi kwa Makapuni ambayo hayajafanya hivyo bado.

“Vyama vya wafanyakazi vinasaidia sana kuleta tija na ufanisi katika maeneo ya kazi maana wafanyakazi hutumia vyombo hivyo kushauriana namna bora ya kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Mhagama

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama aliwataka madereva na wamiliki wa vyombo hivyo kuendelea kuzingatia sheria na kuthamini utu na heshima pande zote mbili, Serikali itachukua hatua kwa yeyote atakayekiuka misingi hiyo.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri mkuu Kazi, Vijna na Ajira Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo yatasaidia kutatua changamoto zilizoibuliwa na madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji.

Mkutano wa wadau wa sekta ya usafirishaji umefanyika Jijini Dodoma ukishirikisha Wizara zinazohusika na masuala ya uchukuzi, Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Vyama vya Wamiliki wa Usafirishaji.