Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

NAIBU WAZIRI UMMY AWAFUNDA VIONGOZI WA VYAMA VYA WATU WENYE ULEMAVU KUSHIRIKIANA NA SERIKALI


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewatanga Viongozi wa Vyama vya Watu wenye Ulemavu kuhakikisha wanashirikiana na Serikali ili waweze kuimarisha ustawi na kuchochea gurudumu la maendeleo ya kundi hilo maalum.

Rai hiyo ameitoa wakati alipokutana na Viongozi wa Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya Temeke lengo ikiwa ni kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu sambamba na kutatua changamoto zinazo wakabili wenye ulemavu nchini.

Mheshimiwa Ummy alieleza kuwa Serikali inawajali na kuthamini wenye ulemavu na katika kulitambua hilo Serikali imekuwa ikishirikiana na asasi za Watu wenye ulemavu kwa nia njema na dhamira ya dhati ili kutetea maslahi ya kundi hilo katika jamii inayowazunguka.

“Mkiwa kama viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu mtambue mnajukumu na ni wajibu wenu kushughulikia masuala mbalimbali ya wenye ulemavu kwa kushirikiana na serikali ili kufanikisha malengo mliyonayo,” alisema Ummy

“Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikitatua matatizo ya wananchi papo kwa papo na ndivyo tulivyoelekezwa sisi watendaji wake kutatua changamoto za wananchi na ndio maana nipo hapa kusikiliza kero zenu na kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Naibu Waziri Ummy

Alieleza kuwa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu wanatakiwa kutambua majukumu yao na wayatekeleze kwa weledi na ufanisi ili waweze kufanikisha masuala mbalimbali yanayowakabili wenye ulemavu.

Aliongeza kuwa Watu wenye Ulemavu wanauwezo wa kufanya miradi mikubwa ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuweza kuajiri wenzao wengine wenye ulemavu, hivyo aliwaasa viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu nchini kuanzisha miradi mikubwa.

Sambamba na hayo Naibu Waziri, amewata Maafisa Ustawi wa Jamii kuongeza juhudi na kasi katika kuhamasisha Watu wenye Ulemavu wananufaika na fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri ya 2% ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Naibu Waziri Ummy ametaka uwepo wa utaratibu mzuri na ambao utakuwa rafiki kwa Watu Wenye Ulemavu kupata mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri pasipo kuwa na vikwazo vyovyote.

“Watu wenye Ulemavu wanapokuja kuomba mikopo hiyo uwepo utaratibu ambao utaharakisha upatikanaji wa mikopo hiyo kwa kuwa kundi hili linahitaji uangalizi maalum tofauti na mikopo iniayotolewa kwa wale wasio na ulemavu,” alieleza Mheshimiwa Ummy

Pia, Mheshimiwa Ummy alitumia fursa hiyo kuvitaka vikundi vya watu wenye ulemavu kuachana na kasumba kuwa mikopo wanayopatiwa na halmashauri ya 2% kuwa ni misaada au inatolewa bure badala yake wakope na kurejesha kwa wakati ili waweze kukopeshwa tena zaidi.

Naibu Waziri Ummy alitumia fursa hiyo kupongeza halmasuari ya Temeke kwa namna ambavyo imekuwa ikiratibu vizuri utoaji wa mikopo ya 4% kwa Wanawake, 4% kwa Vijana na 2% kwa Watu wenye Ulemavu.

Akizungumza kabla, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Godwin Gondwe alieleza kuwa halmashauri ya temeke imekuwa ikishughulikia masuala ya watu wenye ulemavu kupitia dawati la “One Stop Jawabu” na halmashauri hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya asilimia 10 (4% Wanawake, 4% Vijana na 2% Watuwenye Ulemavu) kwa ajili ya kuwainua kiuchumi.

“Utaratibu huu ambao tumekuwa tukiutumia Wilaya ya Temeke umehamasisha wilaya nyingine kuja kujifunza hapa kwetu njia bora tunazozitumia katika kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Gondwe

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke Bw. Lusubilo Mwakabibi alisema kuwa Halmashauri ya Temeke imepokea maelekezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri na wataendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili kundi la wenye Ulemavu.