Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Prime Minister's Office

Labour, Youth, Employment and Persons with Disability

News

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AWATAKA VIJANA KUJIAJIRI


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde amewataka vijana kuondokana na dhana ya kwamba ili waonekane wana ajira lazima wafanye kazi ofisini badala yake amewaasa wajiajiri na kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika hafla iliyowakutanisha vijana zaidi ya 100 Waliochanguliwa kujiunga na programu ya Vijana 2jiajiri inayoratibiwa na Benki ya KCB, alisema kuwa Serikali inatarajia ifikapo mwaka 2025, asilimia 40 ya nguvu kazi ya nchi ambayo ni vijana itakuwa imeajiriwa katika sekta ya viwanda.

Mavunde amesema Serikali inatengeneza mazingira wezeshi kwa vijana yatakayowasaidia kuweza kujiajiri na wengine kuajiriwa na kuongeza kuwa ukuaji wa viwanda nchini utafanikisha jambo hilo.

"Tatizo vijana wengi wanafikra ya kuajiriwa na wanawaza kuwa lazima wavae shati jeupe asubuhi suruali nyeusi na kwenda ofisini, mimi nawaomba mbadilike na ondoeni fikra hiyo kuanzia sasa, mnapaswa kujiajiri kwa kufanya shughuli yoyote inayowaingizia kipato," amesema Mavunde.

Alieleza kuwa pamoja na serikali kutengeneza mazingira hayo ili vijana waweze kuondokana na dhana ya kwamba waonekane wana ajira ni lazima wafanye kazi maofisini badala yake amewataka wahakikishe wanajiajiri.

"Tafiti za mwaka 2014 zinaonesha nguvukazi yenye uwezo wa kufanyakazi ni watu Milioni 24.3 na inaongezeka kila mwaka katika soko la ajira, kwa hiyo wewe kijana ukikaa nyumbani na kujiaminisha kuwa siku moja utaajiriwa Benki au sehemu yoyote ile nikwambie unaendelea Kupoteza muda wako, tambua kuwa ajira haiwezi kukufuata ulipo bali ni kuwa wabunifu katika kuanzisha shughuli za kiuchumi,"

Aidha amesema Serikali ya awamu ya tano inatambua elimu ya ufundi na ndio maana imetenga fedha kwa ajili ya kujenga vyuo vingi vya elimu na ufundi stadi ili wanafunzi wapate elimu na kuweza kujiajiri.

Naye, Kaimu Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) Dar es Salaam, Violet Fumbo amesema programu ya Vijana 2jiajiri inayosimamiwa na Benki ya KCB ni mkombozi kwa vijana wengi kwani itawasaidia kuweza kupata elimu ya ufundi stadi itakayowawezesha waweze kufanyakazi.mbalimbali za ujasiriamali.

Amesema kijana yeyote atakayepata fursa ya kupata elimu ya ufundi na ujasiriamali anapaswa kuondokana na dhana ya kuajiliwa na kuongeza kuwa VETA ipo tayari kushirikiana na KCB ili kuweza kuwasaidia vijana kutimiza malengo yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya KCB,Cosmas Kimario amesema jumla ya Sh. Milioni 80 wamezitoa ili kuwasaidia vijana 123 kuwezakupata elimu ya ufundi stadi katika chuo cha VETA na baadae waweze kujiajiri.