News
Japan kuongeza ubia na Tanzania
Tanzania na Japan zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao, hasa katika maeneo ya maendeleo ya vijana na ukuaji wa uchumi.
Msisitizo huo umewekwa wazi wakati wa mazungumzo kati ya Makamu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Japan, Mheshimiwa Gembá Koichiro, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Ridhwan Jakaya Kikwete yaliyofanyika Dar es salaam Agosti 27 mwaka huu.
Katika mazungumzo hayo Japan imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania katika kuendeleza rasilimali watu kupitia ufadhili wa masomo (scholarships) kwa wanafunzi wa Kitanzania, hasa wale wanaosomea Hisabati na Sayansi, ili kuwajengea uwezo wa kitaalamu na kuchangia katika ukuaji wa taifa.
Pia kubadilishana ujuzi kati ya nchi hizo mbili na kuwafanya vijana wa Tanzania kuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la kisasa la ajira.
Kwa upande wake, Waziri Ridhwan Kikwete alipongeza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan, akisema kuwa umekuwa na faida kubwa ambapo alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inawekeza kwa dhati katika maendeleo ya vijana, akibainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya vijana milioni 30 wenye umri chini ya miaka chini ya 35.
Waziri Kikwete alitaja baadhi ya mafanikio ya serikali katika kuwezesha vijana na watu wenye ulemavu ni pamoja na kupitia Kodi ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL), Tanzania imetoa mafunzo kwa Watanzania 155,195, na kwamba Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umetoa mikopo kwa zaidi ya biashara 1,126 zinazomilikiwa na vijana.
Aidha, alibainisha kuwa serikali imetenga jumla ya ekari 274,047.33 na mita za mraba 540,642 za maeneo ya biashara kwa ajili ya vijana 193,053.
Aidha Mheshimiwa Kikwete alitoa shukrani za dhati kwa Japan kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) kwa msaada wao katika sekta mbalimbali nchini. Pia alizitaja kampuni za Kijapan kama Konoike Construction Company Ltd., Sumitomo Mitsui Construction Company Ltd. na Toyota Tsusho East Africa, kama washirika wa maendeleo wa kutegemewa.